KARIBU KATIKA BLOG HII YA KIFALME. KWA MAWASILIANO: +255715006977

Thursday, April 14, 2011

KITABU CHA ASSOSAA HICHOO SOKONI...

KILE kitabu kilichotokea kuwa gumzo kubwa kabla hakijatoka, cha 'jifunze Lingala' cha nguli wa miondoko ya muziki wa dansi hapa nchini, Tshimanga Kalala Assosaa 'Mtoto Mzuri', kimeingia sokoni leo, imefahamika.
Kwa mujibu wa Assosaa aliyezungumza na mwandishi wa habari hizi, nyumbani kwake Mtaa Mindu, Upanga, jijini Dar es Salaam jana, kitabu hicho kinapatikana sehemu mbalimbali ya mitaa ya miji yote hapa nchini.
Akizungumzia lengo la kutoa kitabu hicho chenye kurasa 56 na ambacho kimesheheni picha na baadhi ya vibao vya wakongwe wa Kongo (DRC), Assosaa alisema kuwa, amekusudia kuwasaidia watangazaji wanaopiga nyimbo za Bolingo bila kufahamu maana yake.
Aidha, Assosaa alieleza kuwa, kadhalika kitabu chake hicho kitakuwa msaada tosha kwa wanamuziki wa dansi wa Kitanzania wanaoimba vibao vya Bolingo pamoja na wale wanaofanya biashara kati ya hapa nchini na Kongo (DRC).
"Hili ni toleo la kwanza la kitabu hiki, ambako baadaye kikishasambaa na kuenea zaidi, nitaanza mkakati wa kutayarisha toleo la pili," alisema Assosaa, kati ya waimbaji mahiri hapa nchini, anayemiliki bendi yake binafsi iitwayo 'Bana Maquiz'.





UNYAYO KUINADI 'ENEMY' KWENYE TV LEO

NYOTA mpya wa muziki wa Kizazi Kipya ‘Bongo Fleva’, Khamis Tambiko ‘Unyayo’ leo anatarajia kuanza kusambaza video ya kibao chake kipya, ‘Enemy’, kwenye vituo mbalimbali vya Televisheni kwa utambulisho.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jijini Dar es Salaam jana, Unyayo alisema kuwa, anaamini video ya kibao chake hicho itawashika mashabiki wengi wa Bongo Fleva kutokana na namna alivyokiandaa vema.
“Video hii naamini itakuwa funika bovu kutokana na kuinakishisha zaidi kwa kumshirikisha mkali wa sanaa ya uchekeshaji hapa nchini, aitwaye ‘Zimwi’,” alisema Unyayo.
Aidha, unyayo alieleza kuwa, baada ya kumaliza kuisambaza video ya kibao hicho kwenye vituo vya televisheni, ataanza kumalizia kuaandaa almbamu nzima itakayokamilika baadaye mwaka huu.

Khamis Tambiko 'Unyayo'

Thursday, April 7, 2011

MWINJUMA MUUMIN AWAAHIDI MAKUBWA MASHABIKI TWANGA...

MWIMBAJI mpya wa bendi ya muziki wa dansi ya African Stars International 'Twanga Pepeta Sugu', Mwinjuma Muumin ameahidi kufanya mambo makubwa akiwa na bendi yake hiyo aliyojiunga nayo hivi karibuni baada ya kuibomoa Bwagamoyo Sound aliyokuwa akiimiliki mwenyewe.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Muumin ambaye ni kati ya waimbaji nguli wanaotikisa vilivyo anga la muziki wa dansi hapa nchini, alisema amekusudia kuwadhihirishia mashabiki pamoja na wapenzi wa Twanga Pepeta kuwa, ametua katika bendi hiyo kikazi zaidi na kwamba hatokuwa na masihara jukwaani.
"Unajua, baadhi ya mashabiki na wapenzi wameshaanza kukubali kuwa, hapa Twanga mimi ndio mahali pangu hasa, ila tatizo limebaki kwa wengine kukosa imani na kuamini kuwa pengine huenda wakati wowote nikawapa kisogo, jambo ambalo binafsi silifikirii kabisa," alisema Muumin.
Aidha, muumin alieleza kuwa, hivi sasa yuko katika mchakato wa kuhakikisha anawapakulia mashabiki vibao motomoto kuanzia kwenye albamu ijayo ya Twanga Pepeta, inayotarajiwa kufyatuliwa hivi karibuni, ambako baadhi ya vibao hivyo tayari vimeshaanza kutumbuizwa kwenye kumbi huku vikiwa na sauti ya nguli huyo.

MAANDALIZI ONYESHO LA JAHAZI MODERN TAARAB, MANCHESTER MUSICA YAANZA KWA MBWEMBWE DAR...

MAANDALIZI ya lile onyesho maalum la pamoja kati ya mabingwa wa mipasho hapa nchini, Jahazi Modern Taarab 'Wana Nakshi Nakshi' na wakali wa miondoko ya muziki wa dansi, Manchester Musica 'Vijana wa Full Vipaji' yameanza kwa kishinndo jijini Dar es Salaam.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Wakurugenzi Wakuu wa makundi hayo, Jarome Mponda (Manchester) na Mzee Yussuf 'Mfalme' (Jahazi) walisema kuwa, wasanii wao wako katika mazoezi makali kujiandaa na onyesho hilo lililopangwa kurindima Mei 8, kwenye ukumbi wa Travertine Hotel, jijini Dar es Salaam.
"Unajua, hii ni mara yetu ya kwanza sisi Wana Jahazi kufanya onyesho la pamoja na Manchester, kwahiyo hatuna budi kufanya mazoezi ya nguvu kuhakikisha kuwa jamaa hawa hawatupigi bao kwa wao kupagawisha zaidi mashabiki zaidi yetu, kwenye ukumbi wetu wenyewe wa nyumbani," alisema Mfalme Yussuf. 
Aidha, Mkurugenzi wa Manchester Musica, Jerome Mponda naye alieleza kuwa, hali iko hivyo pia hata kwao kwani nao wanafanya mazoezi ya kukata na shoka kambini kwao Mbagala Kilungule ili kujiweka sawa na onyesho hilo wakichelea kuzidiwa nguvu na wenzao hao wa Jahazi Modern.

MVUA KIDOGO TU, KIZAA ZAA JIJINI DAR...

MVUA ndogo iliyonyesha jana mchana jijini Dar es Salaam imeonekana kuleta madhara makubwa kwenye baadhi ya maeneo ya jiji hilo lenye wakazi wengi wakiwamo wanamuziki pamoja na wasanii wa fani mbalimbali za burudani hapa nchini.
Kati ya maeneo yaliyokumbwa na zahama la mafuriko yaliyotokana na mvua hizo ni Mtaa wa Soko Mjinga, Mtoni Mtongani, ambako familia kadhaa zilijikuta zikiacha shughuli zao kwa muda na kuanza kazi ya kuondoa maji yaliyovamia vyumbani mwao na kuleta uhalibifu mkubwa wa mali zao.
Mwandishi wetu aliyetembelea eneo la tukio alishuhudia namna hali halisi ilivyokuwa, ambako baadhi ya wakazi waliitupia lawama Halimashauri ya Manispaa kwa kupanga miundo mbinu mibovu ya barabara zenye mitaro yenye uwezo usiolingana na msongo wa maji pindi mvua zinapoandama.
"Unajua, hii yote visingetokea iwapo Manispaa ingerekebisha vema miundombinu yake, lakini wapi bwana, hawa jamaa sijui hela wanazipeleka wapi halafu wanatutengenezea barabara katika mtindo wa 'bora liende'," alisema Mohammed Mauji, mmoja wa wacharazaji gitaa kiongozi la Solo wa Jahazi Modern Taarab. 

 Mohammed Mauji

Moja ya nyumba iliyokumbwa na balaa la mafuriko jana huko Mtaa wa Soko Mjinga, Mtoni Mtongani jijini Dar es Salaam.

 Maji yakiwa yameacha mkondo wa mfereji uliojengwa kando ya barabara na kusambaa kwenye makazi ya watu
 Msichana akiokota baadhi ya viwalo vilivyokuwa vimesombwa na maji katika mafuriko hayo

Hapa ni mahali mfereji mmoja mdogo unapopokea maji kutoka katika mifereji mingine miwili mikubwa zaidi!!!

ZENA KUONEKANA TENA KWENYE 'POISON OF LOVE'
   
Na Abdallah Menssah
NYOTA wa kike wa tasnia ya filamu hapa nchini, Annan Shaaban ‘Zena’ hivi karibuni anatarajia kuanza kuonekana kwenye filamu mpya ya kwake mwenyewe, inayokwenda kwa jina la ‘Poison of Love’.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jijini Dar es Salaam jana, Zena alisema kuwa, katika filamu hiyo iliyobeba ujumbe mzito juu ya athari za usiri na wasiwasi katika mapenzi, ameigiza kama Mhusika Mkuu akitumia jina la ‘Nina’.
“Baadhi ya nyota wengine niliowashirikisha katika filamu hiyo ambayo kiukweli naamini itakuwa moto wa kuoteambali kutokana na namna ninavyoiandaa ni Tazan, Tonny, Mzee Magali pamoja na Bi Mjata,” alisema Zena.
Aidha, Zena alieleza kuwa, filamu hiyo ambayo kwa sasa iko katika hatua ya uhariri kwenye Studio iitwayo ‘Yangu Vision’ iliyo chini ya Wilblod Antony, ambako baada ya baada wiki mbili itakuwa sokoni ikipatikana kwenye mikanda ya kawaida, VHS, VCD pamoja na DVD.    
Kabla ya filamu hii, Zena alitikisa kwenye makundi kama ‘Hisia Connection’ na Jakaya Theatre alikoshiriki Tamthilia kadhaa ikiwamo ile ya ‘Kizunguzungu’ iliyokuwa ikirushwa kwenye runinga ya ITV, alishiriki kucheza filamu ya ‘Saturday Morning’.
Tanzania Daima Ijumaa, Aprili 8, 2011.

Annan Shaaban 'Zena'

FILAMU MPYA YA JB HIYOOO...

FILAMU mpya iliyotokea kujizolea umaarufu mkubwa kabla haijatoka, inayokwenda kwa jina la ‘Senior Bachelor’, inatarajiwa kutinga sokoni Jumatatu, Aprili 18, mwaka huu ambako itapatikana kwenye mikanda ya kawaida, VHS, VCD pamoja na DVD.
Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Jerusalem Film Company, Jacob Stephen ‘JB’ alimweleza mwandishi wa habari hizi jijini Dar es Salaam jana kuwa, filamu hiyo imebeba ujumbe mzito kwa jamii kwa kuanika upande wa pili wa maisha ya Mapedeshee.
“Unajua, filamu yangu hii mpya imewamulika Mapedeshee na maisha yao kwa ujumla, kwani wengi wao hupenda kuonyesha ufahari na kumwaga pesa kwenye majumba ya starehe, wakati kumbe hata pa kulala hawana na mwishowe hutokea kujikuta wakifia katika nyumba za wageni,” alisema JB.
Aidha, JB alisema, katika filamu hiyo ya pili kutolewa na Kampuni yake kwa mwaka huu, amecheza yeye mwenyewe pamoja na nyota wengine kadhaa wa maigizo kama Jack wa Chuzi, Jackline Uwoya na mkongwe wa muziki kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Bozi Boziana.

Wednesday, April 6, 2011

USIPITWE...

Burudani kama hii...

Ni kila Jumapili pale Travertine Hotel Magomeni...

Njoo ukutane na Malkia Leyla Rashid na wengineo

PATA UHONDO...!!!

Taarifa za kuwa, mkali wa kike wa Bongo Fleva, Stara Thomas ameamua kuachana na muziki wa aina hiyo na kuanza kujihusisha na miondoko ya Injili inaonekana kuwashitua wengi, lakini ndio hivyo tena, Stara na Bongo Fleva kwa sasa ni kama chui na paka.

Hapa akiwa na mtoto wake aitwaye Jazz, katika pozi la aina yao

Jamani mmemuona nyota mpya wa Bongo Fleva huyoooo, anaitwa Linah... ni hatari lakini salama
Hebu cheki pozi lake kwanza!!!

Hapa nilikuwa namsaidia kuimba kibao 'Njiwa Peleka Salamu', hii ilikuwa ni siku moja kabla ya siku ilee zilipotolewa Tuzo za Kili pale Diamond Jubilee, 2011.

Huyu ni mmoja wa walee wakung'utaji mahiri wa gitaa zito la Besi katika kundi bingwa la mipasho, Jahazi Modern Taarab, anaitwa Shomari Zizzou akiwa kazini, katika moja ya maonyesho ya kundi lake hilo.

Tuesday, April 5, 2011

KWA WAPENZI WA BURUDANI TUU!

Hii ni Pub bab' kubwa inayosifika kwa kuwa na huduma za kisasa kabisa, yenyewe iko maeneo ya Mbagala Kilungule jijini Dar es Salaam. Kati ya vinywaji vinywaji bomba vinavyopatikana kwenye Pub hii ni ile pombe ya ajab ambayo ukiiwasha kiberiti inawaka kama Petroli, iitwayo 'SAMBUKA'. 

Mkung'utaji mahiri wa gitaa Kiongozi la Solo wa wakali wa miondoko ya dansi, Manchester Musica, Adam Hassan ameweka wazi kuwa, hana mpango wa kurejea katika bendi yake ya zamani ya Extra Bongo 'Next Level'.
Akizungumza katika ofisi za Blog hii, jijini Dar es Salaam jana, Adam alisema hana mpango wa kurejea Extra Bongo kutokana na kuwa, kipato anachokipata sasa akiwa na bendi ya Manchester Musica kinakidhi mahitaji yake yote muhimu.
Aidha, Adam alisema kuwa, kinachomfanya aweke nadhiri ya kutorejea tena katika bendi hiyo inayoongozwa na Ally Choki ni mkakati wake wa kuhakikisha anafanya maisha kwa ajili ya pesa na si kujituma kwa manufaa ya 'kumnenepesha shetani wakati kiti anakonda'.
Hivi sasa Adam ndiye Kiongozi Mkuu wa bendi hiyo ya Manchester inayoundwa na wanamuziki wengi chipukizi lakini wenye umahiri wa hali ya juu katika kurindimisha burudani ya dansi hapa nchini.

MWANAMIPASHO wa kundi la Dar es Salaam Modern Taarab, Ammar Sultan ameamua kutoka kivingine kwa kuachia kibao kilicho katika miondoko ya muziki wa Kizazi Kipya 'Bongo Fleva' kinachokwenda kwa jina la 'Nampenda Albino'.
Akizungumza katika ofisi za Blog hii jijini Dar es Salaam jana, Ammar alisema kuwa, kibao hicho amekirekodia katika Studio ya White Production iliyo chini ya mtayarishaji mashuhuri na maarufu hapa nchini, Stive White.
Aidha, Ammar aliyetumia jina la 'Simba Mtoto' katika kibao hicho, alieleza kuwa amejaribu kuchanganya ladha kwa kumshirikisha msanii mwingine wa miondoko hiyo ya Bongo Fleva, anayefahamika zaidi kwa jina la Mamba Mzee.
"Natarajia kuanza kukisambaza kibao hicho kwenye vituo mbalimbali vya radio hapa nchini mwanzoni mwa wiki ijayo kwa utambulisho rasmi kwa wapenzi pamoja na mashabiki wangu," alisema Ammar aliyeimba kibao 'Toto la Afrika' akiwa na Dar Modern.



Na Abdallah Menssah
MWIMBAJI mpya wa bendi ya muziki wa dansi, Joseph Venas ‘Wera Baba’ ameonekana kuwa kivutio kikubwa kwa mashabiki, katika maonyesho yao mbalimbali tangu alipojiunga rasmi na bendi hiyo majuma mawili yaliyopita.
Mwandishi wa habari hizi aliyehudhuria karibu maonyesho yote ya Manchester Musica, toka kujiunga kwa Wera Baba, alishuhudia namna mwimbaji huyo anavyoshangiliwa na mashabiki pamoja na wapenzi wa dansi kila anapopanda jukwaani kuimba.
Baadhi ya vibao vya Manchester Musica ambavyo, Wera Baba aliyejiunga na bendi hiyo akitokea Bwagamoyo Sound iliyokuwa chini ya Mwinjuma Muumin, anaviimba kwa ustadi mkubwa ni pamoja na ‘Pesa’, ‘Sina’, ‘Kijumbe wa Mtaa’, ‘Urithi wa Baba’, ‘Jackline’ na Haraka Haraka za Maisha’.
Katika mazungumzo yake na mwandishi wa habari hizi jijini Dar es Salaam jana, Wera Baba alisema, amedhamiria kuwadhihirishia mashabiki wa Manchester Musica kuwa amejiunga na bendi hiyo ili kuiongezea makali na kuifanya iwe tishio zaidi. 
“Hivi sasa niko katika mchakato wa hatua za mwanzo za maandalizi kibao changu cha kwanza ndani ya Manchester, kitakachoitwa ‘Dakika za Majeruhi’, ambacho nawahakikishia wapenzi pamoja na mashabiki kuwa kitakuwa funika bovu,” alisema Wera Baba. 

Nyota wa filamu na maigizo hapa nchini, anayefahamika kwa jina maarufu la 'Bambucha' anasema yuko tayari kuigiza katika Kampuni yoyote atakayofika nayo mkataba kuanzia sasa.
Bambucha alisema kuwa, amefikia uamuzi huo baada ya kubaini kuwa Kampuni nyingi zimekuwa zikihitaji kufanya naye muvi za Kibongo.
Huyu ni Mkurugenzi wa bendi maarufu ya muziki wa dansi, Manchester Musica ambayo hivi sasa inakuja juu kwa kasi kwelikweli katika medani hiyo.


Huyu naye ni Chid Benz katika pozi la aina yake kama alivyonaswa hivi karibuni.
Huyu ni mtayarishaji maarufu wa filamu za Kibongo, Omary Mbega maarufu kama 'Director Ommy'

Chid Benz na Banana Zoro katika picha ya pamoja

Saturday, April 2, 2011

UMEIPATA HII...?

KAMPUNI inayojihusisha na ukuzaji vipaji vya wasanii nchini, Twins Art Production keshokutwa Jumatatu inatarajia kufungua Studio ya kurekodia muziki itakayojulikana kama ‘Twins Records’.
Meneja Mkuu wa Twins Art, Daud Juma Mwandalima aliiambia Blog hii jijini Dar es Salaam jana kuwa, Studio hiyo itakuwa ikirekodi kazi mbalimbali za wasanii wa muziki.
Aidha, Mwandalima alieleza kuwa, Studio hiyo ambayo Mkurugenzi Mkuu wake ni Vick Kanyoka, itakuwa vilevile ikiandaa matamasha pamoja na kuwasaidia wasanii walio katika mazingira magumu.
“Pia tutakuwa na kikundi cha wasanii mahiri ambao kazi yao itakuwa ni kurekodi matangazo ya kibiashara kwenye Kampuni mbalimbali tutakazokubaliana nazo, ndani na nje ya nchi,” alisema Mwandalima.